Swahili Protective Orders

​Taarifa ya Amri za Ulinzi

Taarifa hii ilichukuliwa kutoka kwenye kijitabu cha "How to Obtain a Protective Order" kilichochapishwa na Ofisi ya Utawala ya Mahakama. Ni mwongozo wa namna ya kupata amri za kiraia kwa wale wanaotafuta ulinzi dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa majumbani, ukatili na unyanyasaji wa kimapenzi, kunyemelea na shambulio la kingono.

Tafadhali kumbuka kwamba mlalamikaji ni mtu ambaye anawasilisha ombi kwa ajili ya amri ya ulinzi. Mshtakiwa ni mtu ambaye anatuhumiwa kufanya unyanyasaji.

Kwa nini uwasilishe EPO au IPO?

Kustahiki kuwasilisha EPO au IPO, mshtakiwa lazima awe amefanya moja kati ya:

  • Amekujeruhi au amekushambulia kimwili.
  • Amekubaka.
  • Amekufanyia unyanyasaji wa kingono au amekushambulia kingono.
  • Amekutishia kukujeruhi au kukufanyia shambulio la kimwili.
  • Amekunyemelea.
  • Amefanya jambo ambalo limekufanya uhofie majeraha madogo ya mwili, majeraha makubwa ya mwili, unyanyasaji wa kijinsia, kukabwa au shambulio.

Aina za Amri za Ulinzi

Mahakama inaweza kutoa amri ya ulinzi kwa muathirika wa ukatili wa majumbani, ukatili na unyanyasaji wa kimapenzi, kunyemelea na/au shambulio la kingono. Mashauri ya amri za ulinzi ni tofauti na mashauri ya jinai. Amri za ulinzi zinalenga kuzuia matendo ya baadaye ya ukatili na unyanyasaji. Shauri la jinai kwa kawaida hushughulikiwa na mwanasheria wa wilaya, ambaye humshtaki mshtakiwa kwa matendo ya ukatili na unyanyasaji ambayo tayari yamefanyika.

Amri za Ulinzi za Muda Mfupi. Mahakama inaweza kutoa amri ya dharura ya ulinzi (EPO) katika mashauri ya ukatili wa majumbani au amri ya ulinzi ya mtu na mtu ya muda mfupi (TIPO) katika mashauri ya ukatili wa kimapenzi na unyemeleaji/shambulio la kingono. Hizi ni amri za muda mfupi zinazolenga kuzuia ukatili na unyanyasaji kwa kuweka vikwazo kwenye matendo ya mshtakiwa hadi usikilizaji wa mashauri ufanywe na mahakama, kwa kawaida ndani ya siku 14.

Amri za Ulinzi za Muda Mrefu. Amri za ukatili wa majumbani (DVO) na amri za ulinzi kati ya mtu na mtu (IPO) zinaweza kudumu hadi miaka mitatu. Amri hizi zinalenga kuzuia unyanyasaji na ukatili kwa kumwekea vikwazo mshtakiwa baada ya usikilizaji wa shauri mahakamani.

Je, nani anaweza kupata amri ya ulinzi?

Ili kupata amri ya ulinzi, wahusika lazima wawe na uhusiano unaostahiki. Uhusiano unaostahiki ni pamoja na:

  • Wanafamilia. Hii inajumuisha mwenza, mwenza wa zamani, mzazi, mtoto, mtoto wa kambo, babu/bibi, mjukuu, au mtu mwingine yeyote anayeishi katika kaya hiyihiyo kama mtoto ikiwa mtoto huyo ndiye anayedaiwa kuathirika.
  • Jamaa wa wenza ambao hawajaoana. Hii inajumuisha jamaa wa wenza ambao hawajaoana ambao wanadaiwa kuwa na mtoto pamoja, watoto wowote wa wenza hao, au jamaa wa wenza ambao hawajaoana ambao wanaishi pamoja au waliishi pamoja hapo kabla.
  • Uhusiano wa uchumba kati ya watu wawili ambao wana au walikuwa na uhusiano wa kimapenzi au wa uhusiano wa karibu.
  • Mwathirika wa kunyemelea au shambulio la kingono.

Je, nani anaweza kulindwa? 

  • Unaweza kuomba ulinzi kwa ajili yako mwenyewe, watoto wako na/au watu wengine ambao unadhani wanaweza kuhitaji ulinzi.
  • Kama wewe ni mtu mzima na unadhani mtoto anahitaji ulinzi lakini wewe huhitaji, unaweza kuwasilisha ombi kwa niaba ya mtoto huyo.
  • Ikiwa una umri chini ya miaka 18, mtu mzima anaweza kuwasilisha ombi kwa niaba yako.

Je, wapi ninaweza kuwasilisha ombi la amri ya ulinzi?

Kuwasilisha ombi la amri ya ulinzi, tembelea Ofisi ya Karani wa Mahakama kwenye wilaya ya nyumbani au kwenye wilaya ambayo unaishi kwa sasa ikiwa umeondoka nyumbani kwako ili kukimbia unyanyasaji.

Kuna Ofisi ya Karani wa Mahakama katika kila wilaya za Kentucky.

Unaweza kupata taarifa za mawasiliano ya Karani wa Mahakama hapa.

  • Unaweza kupata amri ya ulinzi saa 24 kwa siku.
  • Hakuna ada au gharama za kuwasilisha ombi.
  • Baada ya muda wa kazi, unapaswa kuwasiliana na afisa usalama wa mahali ulipo kwa msaada wa kupata amri ya ulinzi.

Je, ninajazaje ombi?

Utaombwa kutoa taarifa zako na za mshtakiwa. Ni muhimu kutoa taarifa nyingi za mshtakiwa kadri iwezekanavyo – kama vile tarehe ya kuzaliwa, namba ya Hifadhi ya Jamii na anwani – ili aweze kupewa amri yoyote inayoweza kutolewa. Anwani yako na tarehe ya kuzaliwa zitakuwa siri.

Utaombwa uorodheshe watoto wowote ambao wewe na mshtakiwa mnao, na unaweza kuomba kwamba watoto hawa walindwe na amri yoyote inayoweza kutolewa.

Chini ya "Pendekezo la Unafuu", unaweza kuomba ulinzi ambao unadhani unafaa katika mazingira yako. Utatakiwa uape kwamba taarifa ulizotoa ni sahihi.

Je, nini kitatokea baada ya ombi kuwasilishwa?

Ombi litawasilishwa haraka kwa hakimu au kamishna wa mashtaka kwa ajili ya mapitio.  Ikiwa hakimu atatoa EPO, TIPO au wito, usikilizaji wa shauri utapangwa ndani ya siku 14 ili kuamua kama amri ya muda mrefu inahitajika. Utapewa kitu ambacho kitakuonyesha tarehe na muda wa usikilizaji wa shauri. Ikiwa hufahamu siku iliyopangwa kwa ajili ya usikilizaji wa shauri, wasiliana na Ofisi ya Karani wa Mahakama.

Afisa usalama atajaribu kumpatia amri ya ulinzi au wito mshtakiwa. Amri ya ulinzi haiwezi kufanya kazi hadi mshtakiwa atakapopewa nakala ya amri au atakapojulishwa kuhusu amri ya ulinzi na afisa usalama. Unaweza kuwasiliana na "agency assigned service" (aliyeorodheshwa kwenye amri) ili kujua kama mshtakiwa amepewa nakala.

Amri ya ulinzi (EPO/TIPO) itafanya kazi hadi pale usikilizaji wa shauri mahakamani umefanyika, kwa kawaida ndani ya siku 14. Kama mshtakiwa hajapewa EPO/TIPO, amri itaendelea hadi huduma itakapotekelezwa (hadi miezi sita) au hadi pale amri itakapoondolewa  na mahakama. Hata kama unadhani huhitaji tena ulinzi, utatakiwa uhudhurie siku iliyopangwa ya usikilizaji wa shauri mahakamani.

Hakimu pekee ndiye anayeweza kutoa tarehe mpya ya mahakama au kubadili amri. Kuliongana na hali za shauri, mahakama inaweza kukupa udhuru wa kuhudhuria mahakamani siku zijazo hadi pale mshtakiwa atakapopewa nakala. Kama EPO/TIPO haijatolewa kwa hadi miezi sita, utapokea tangazo kutoka mahakamani kwenye anwani yako iliyokuwa inafahamika awali ili kukujulisha kwamba amri inakaribia kwisha na kwamba utatakiwa kuja kwenye Ofisi ya Karani wa Mahakama ili kujaza ombi jipya ili kuendelea na shauri.

Je, unapaswa kuja na vitu gani kwenye usikilizaji wa shauri?

Huu unaweza kuwa usikilizaji pekee wa shauri, hivyo unapaswa kuja na mashahidi wowote ulio nao na hati zozote ambazo zinaweza kuwa ushahidi wa kile kilichotokea, kama vile ripoti za polisi, picha na hati za matibabu. Karani wa mahakama anaweza kukupatia fomu kwa ajili ya hati ya kuitwa mahakamani kwa mashahidi wowote.

Ikiwa unaomba msaada wa mtoto, leta muhtasari wa malipo na marejesho ya kodi kama inawezekana. Taarifa zote hizi zitakuwa moja ya kumbukumbu ya mahakama.

Je, nini kinaweza kutokea katika usikilizaji wa shauri?

Katika usikilizaji kamili wa shauri, mahakama itasikiliza ushahidi kutoka kwako, kwa mshtakiwa na mashahidi wengine wowote. Mahakama inaweza kutupilia mbali shauri au kutoa DVO au IPO (amri ya ukatili wa majumbani au amri ya ulinzi wa mtu binafsi), ambayo inaweza kujumuisha masharti yafuatayo:

  1. Kumuamuru mshtakiwa kutowasiliana na wewe au na watu wengine isipokuwa kama ilivyoelekezwa na hakimu.
  2. Kumuamuru mshtakiwa kutoenda karibu na makazi fulani, shule au sehemu ya kazi ya mlalamikaji.

KUMBUKA: Hili lazima liombwe kwenye ombi la amri ya ulinzi. Taarifa yoyote ya anwani iliyotolewa si siri na itaonekana kwa mshtakiwa.

  1. Kumuamuru mshtakiwa kutokunyanyasa wala kukutisha.
  2. Kumuamuru mshtakiwa kutoharibu wala kutozitupa mali zako.
  3. Kumuamuru mshtakiwa kuondoka kwenye makazi yako.
  4. Kutoa uangalizi wa watoto wa muda mfupi.
  5. Kutoa msaada kwa mtoto.
  6. Kutoa amri ya ushauri.
  7. Kitu chochote kile kinachohitajika kukomesha vitendo vya ukatili baadaye.

Unapaswa kusoma kwa makini amri zote unazopata. Ikiwa una maswali kuhusu kile amri yako inamaanisha, wasiliana na mwanasheria wako (kama unae), mpango wa ukatili wa majumbani wa mahali husika au wakili wa mwathirika.

Nini kitatokea ikiwa mshtakiwa atakiuka amri ya ulinzi?

Amri ya ulinzi inaweza kutekelezwa katika wilaya yoyote ya jimbo la Kentucky.  Majimbo mengine yanaweza kutekeleza amri, lakini inapaswa kusajiliwa katika jimbo lolote ambalo utahamia au unapanga kuishi kwa muda mrefu.

Ikiwa mshtakiwa atakiuka amri ya ulinzi, machaguo yako yanaweza kujumuisha:

  • Kuwapigia simu polisi, ambao wanaweza kumkamata mshtakiwa.
  • Kurudi kwenye mahakama ambayo ilitoa amri ya ulinzi kuomba kwamba mshtakiwa akamatwe kwa dharau ya kukiuka amri hiyo.
  • Kurudi kwenye Ofisi ya mwanasheria wa wilaya kuangalia kama mshtakiwa anaweza kushtakiwa kwa kosa la kukiuka amri ya ulinzi.

Ufuatiliaji wa GPS. Ikiwa wilaya yako ina huduma ya ufuatiliaji ya mfumo wa upangaji ulimwengu (GPS) iliyopo, unaweza kuiomba mahakama kumuamuru mshtakiwa kuvaa kifaa cha ufuatiliaji wa GPS. Unaweza kufanya hivyo kwa kuwasilisha fomu ya pendekezo mahakamani. Unaweza kuomba fomu hiyo kwenye Ofisi ya Karani wa Mahakama.

Hakimu ataamua kama kumekuwa na ukiukaji hasa uliofanywa na mshtakiwa ambao ulihusisha kutokea au kutishia usalama wako wewe, familia yako au mali zako. Ikiwa hakimu atamuamuru mshtakiwa kuvaa kifaa cha ufuatiliaji, mshtakiwa ataamurishwa kulipia gharama za ufuatiliaji na anaweza kutakiwa kukivaa kifaa ilimradi amri ya ulinzi inafanya kazi.

Ikiwa baadaye utadhani kuwa si muhimu tena, unaweza kuomba kwamba matakwa ya mfumo wa ufuatiliaji GPS yaondolewe.

Je, ninawezaje kubadilisha au kurefusha amri ya ulinzi?

Ikiwa unahitaji kubadilisha masharti ya amri ya ulinzi, lazima uwasilishe pendekezo la mabadiliko kwenye Ofisi ya Karani wa Mahakama katika wilaya ambayo ulipata amri yako ya ulinzi. Upande wowote unaweza kuwasilisha pendekezo la kurekebisha amri. Kisha hakimu atapitia pendekezo na kufanya uamuzi. Hakimu pekee ndiye anayeweza kubadili baadhi au masharti yote ya amri.

Ikiwa unataka amri ya ulinzi kuongezwa zaidi ya tarehe yake ya mwisho, ni lazima uwasilishe pendekezo mahakamani ambalo linaeleza sababu yako (zako) ya ombi hilo. Pendekezo lazima liwasilishwe kabla ya amri kwisha.

Ikiwa mshtakiwa ameamurishwa kuvaa kifaa cha kufuatilia GPS, unaweza kuomba takwa hilo kurefushwa pia.

Je, ninawezaje kupata huduma za msaada?

Nakala ya ombi na amri ya ulinzi vitatumwa kwenda kwenye Baraza la Kentucky la Huduma za Afya na Familia (CHFS) na kuelekezwa kwenda ama kwenye Mamlaka ya Huduma za Ulinzi wa Watu Wazima au Mamlaka ya Huduma za Ulinzi wa Mtoto. Mfanyakazi wa ustawi wa jamii kutoka CHFS anaweza kuwasiliana na wewe ili kukupa huduma za msaada. Kufahamu zaidi, bofya hapa.

Huduma za Kentucky VINE (Taarifa za Mwathirika na Arifa za Kila Siku) zinakupatia ufikiaji wa taarifa na arifa kuhusu amri yako ya ulinzi. Hii inajumuisha kama amri imetolewa, tarehe za usikilizaji kesi, na taarifa kuhusu masharti na vigezo vya amri. Kwa taarifa zaidi kuhusu huduma za VINE, bofya hapa. Kufahamu jinsi ya kusajili amri yako ya ulinzi, piga simu 877-687-6818 au bofya hapa.

Huduma za waathirika pia zinapatikana katika jimbo la Kentucky.  Kwa taarifa zaidi, piga simu ya bure kwa Namba ya Kitaifa ya Ukatili wa Majumbani 800-799-7233, au bofya hapa.

Je, haki zangu ni zipi chini ya Sheria ya Mwenye Nyumba/Mpangaji?

Ikiwa una amri ya ulinzi iliyotolewa na hakimu, basi unaweza kuwa na haki za ziada chini ya Sheria ya Mwenye Nyumba/Mpangaji, ambayo ilianza kufanya kazi tarehe 29 Juni 2017.

Haki hizi zinatumika tu kwenye mikataba ya upangishaji au ya kupanga iliyoingiwa, au iliyohuishwa, mnamo au baada ya tarehe 29 Juni 2017. Unaweza kutaka kushauriana na mwanasheria au wakili wa mwathirika kwa taarifa za ziada kuhusu haki zako chini ya Sheria ya Mwenye Nyumba/Mpangaji.

Haki Chini ya Amri ya Ulinzi ya Muda Mfupi au Amri ya Kutowasiliana

Ikiwa una amri ya ulinzi ya muda mfupi (EPO au TIPO) iliyotolewa au amri ya kutowasiliana iliyotolewa na hakimu kwa mujibu wa KRS  431.064 (shambulio, unyanyashaji wa kingono au ukiukaji wa amri ya ulinzi), una haki zifuatazo:

  • Mwenye nyumba hawezi kutamatisha au kushindwa kuhuisha, au kukataa kuingia mkataba wa upangishaji au kodi na wewe (au vinginevyo kukulipiza kisasi) kulingana na matendo ambayo yamekusababishia kupata amri ya ulinzi ya muda mfupi au kulingana na matendo yoyote ambayo yalitokea wakati wa ukiukwaji wa amri ya ulinzi ya muda mfupi.
  • Unaweza kubadilisha ufunguo ya kitasa au kubadilisha kitasa chenye ubora uleule wa kitasa au ubora mzuri zaidi. Kwanza, lazima umjulishe mmiliki wa nyumba yako kwamba unadhamiria kubadilisha kitasa na umpatie ufunguo kama atakuomba.

Pia mwenye nyumba anaweza kukataa kutoa ufunguo wa kitasa kipya kwa mshtakiwa hata kama pia ameorodheshwa kwenye mkataba wa upangishaji au wa kupanga.

Amri za Ulinzi za Muda Mrefu na Utamatishaji wa Mkataba wa Upangishaji

Zaidi ya haki chini ya amri ya ulinzi ya muda mfupi, mara baada kutolewa kwa DVO au IPO halali dhidi ya mshtakiwa kwa ajili ya ulinzi wako au ulinzi wa mtoto mdogo kwenye kaya yako, unaweza kutamatisha mkataba wa upangishaji au wa kupanga.

Hii haitumiki ikiwa una amri ya ulinzi ya muda mfupi pekee (EPO au TIPO) au amri ya kutowasiliana kwa mujibu wa KRS 431.064. Lazima uwe umepata amri ya ulinzi ya muda mrefu halali (DVO au IPO) kutolewa.

Hii inatumika pekee kwenye mikataba ya upangishaji au kupanga iliyoingiwa au iliyohuishwa mnamo au baada ya tarehe 29 Juni 2017.

Amri ya Ulinzi ya Muda Mrefu Iliyopatikana Baada ya Kuingia Katika au Kuhuisha Mkataba wa Upangishaji au Kupanga

Ikiwa ulipata amri yako halali ya ulinzi baada ya kuingia katika au kuhuisha mkataba wako wa upangishaji au wa kupanga, basi unaweza kutamatisha mkataba wako kwa kwa kumpatia mwenye nyumba wako: 

  • Tangazo la maandishi la utamatishaji ambao lazima uwe na tarehe ya kuanza kutumika kwenye tangazo. Tarehe ya kuanza kutumika lazima iwe angalau siku 30 baada ya mwenye nyumba kupokea tangazo hilo.
  • Nakala ya amri ya ulinzi halali.

Amri za Ulinzi za Muda Mrefu Zilizopatikana Kabla ya Kuingia Kwenye au

Kuhuisha Mkataba wa Upangishaji au wa Kupanga

Ikiwa ulipata amri yako halali ya ulinzi kabla ya kuingia kwenye au kuhuisha mkataba wa upangishaji au wa kupanga, basi unaweza kutamatisha mkataba wako kwa kutoa kwa mwenye nyumba wako:

  • Tangazo la maandishi la utamatishaji ambao lazima uwe na tarehe ya kuanza kutumika kwenye tangazo. Tarehe ya kuanza kutumika lazima iwe angalau siku 30 baada ya mwenye nyumba kupokea tangazo hilo.
  • Nakala ya amri ya ulinzi halali.
  • Tatizo la usalama wako lililoongezeka baada ya kuingia au kuhuisha mkataba wa upangishaji au kupanga.

Utamatishaji wa Upangishaji

Mara baada ya mkataba wa upangishaji au wa kupanga kutamatishwa:

  • Utawajibika tu kisheria kulipa kodi iliyo kwenye mkataba wako wa upangishaji au wa kupanga hadi tarehe ya utamatishaji itakapofika.
  • Hutapata sifa mbaya, kuambiwa una tabia mbaya, au kuwajibika kisheria kulipa nyongeza ya kodi au ada kwa sababu tu ya utamatishaji wa mapema wa mkataba wa upangishaji au wa kupanga.
  • Ikiwa mkataba wako wa upangishaji au wa kupanga utatamatishwa angalau siku 14 kabla ya kuhamia, basi hutatakiwa kulipia uharibifu au adhabu.

PDF inayopakulika hapa:

AOC-275.1 Ombi/Pendekezo la Amri ya Ulinzi

AOC-275.6 Pendekezo la Kurekebisha Amri ya Awali ya Ulinzi

Jinsi ya Kupata Amri ya Ulinzi